WAKABILIANO YAZUKA MSIKITINI YERUSALEM
Fujo zimezuka katika msikiti wa al-Aqsa, Jerusalem Mashariki baada ya polisi wa Israel kuingia eneo la msikiti huo.
Polisi wanasema wameingia “kuzuia ghasia”. Wanadaiwa kutumia gesi ya kutoa machozi na guruneti za kudhibiti waandamanaji. Walishambuliwa kwa mawe na fataki.
Makabiliano sawa na hayo yalishuhudiwa mwishoni mwa mwezi Julai.
Al-Aqsa ni moja ya maeneo matakatifu zaidi miongoni mwa Waislamu na msikiti huo umo eneo la Temple Mount/Haram al-Sharif ambalo pia ni takatifu kwa Wayahudi.
Eneo hilo limekuwa kiini cha mizozo ya kidini na kisiasa kati ya Israel na Wapalestina na hushuhudia makabiliano ya mara kwa mara.
Maafisa wa polisi walikuwa pia wakiwasaka Wapalestina kadha wanaodaiwa kuficha vilipuzi
Jerusalem Mashariki, kwa mujibu wa gazeti la Jerusalem Post.
Washukiwa hao walikuwa wametorokea msikiti wa al-Aqsa na kujificha humo ndani, kwa mujibu wa gazeti hilo.
Mapigano hayo yametokea saa chache kabla ya kuanza kwa Mwaka Mpya wa Kiyahudi, Rosh Hashanah.
Waziri wa Usalama wa Umma Gilad Erdan aliambia gazeti hilo la Post kwamba Wayahudi wanaruhusiwa kuingia kusherehekea Rosh Hashanah, sherehe zitakazoanza Jumapili baada ya jua kutua na kuendelea hadi Jumanne jioni.
Hali ya wasiwasi ilikuwa imetanda jijini humo tangu Waziri wa Ulinzi wa Israel Moshe Yaalon kupiga marufuku makundi mawili ya Kiislamu yaliyokuwa yakikabili Wayahudi waliokuwa wakitembelea eneo hilo.
Bw Yaalon alisema makundi hayo yamekuwa yakichangia kuongezeka kwa wasiwasi na ghasia eneo hilo na ilifaa kuyapiga marufuku ili kudumisha utulivu.
No comments
COMMENT