MWALIMU ALIYE KATAA UCHAWI SASA MBARIKIWA
Mwalimu wa shule aliyeuawa nchini Afrika Kusini kwa kukataa uchawi ametawazwa kuwa mbarikiwa.
Benedict Daswa ndiye mtu wa kwanza kabisa kufikia hatua hiyo kuu katika safari ya kuwa mtakatifu katika kanisa Katoliki eneo la kusini mwa Afrika.
Mwalimu huyo alitawazwa “mbarikiwa” kupitia barua ya kidini iliyosomwa kwa niaba ya Papa Francis na Kadinali Mwitaliano Angelo Amato wakati wa ibada ya misa iliyohudhuriwa na takriban watu 30,000 kijijini Tshitanini, karibu na alikoishi Daswa mkoa wa Limpopo kaskazini mwa taifa hilo.
Waliohudhuria walishangilia sana na kupuliza baragumu.
Daswa alipigwa hadi kufa na wanakijiji wenzake miaka 25 iliyopita alipokataa kumlipa mchawi aliyeahidi kusitisha upepo mkali uliokuwa ukitatiza eneo hilo na kusababisha uharibifu mkubwa.
Mwanzo alipigwa mawe na wanakijiji hao waliokuwa na hamaki. Baada yake kukimbilia nyumba moja, aliandamwa na kupigwa kwa vijiti na pia akamwagiwa maji yaliyokuwa yakichemka masikioni na puani.
Haya yote yalijiri Februari 2, 1990 siku ambayo utawala wa ubaguzi wa rangi nchini humo ulitangaza ungemwachilia huru Nelson Mandela.
"Alipokuwa akiuawa aliomba hadi dakika ya mwisho,” wasifu wake uliosomwa wakati wa ibada hiyo unasema.
Siku yake kuu itakuwa ikiadhimishwa Februari 1.
Takriban asilimia nane ya raia Afrika Kusini ni Wakatoliki.
Papa Francis, aliyetangaza Januari kuwa Daswa angefanywa mbarikiwa, alimsifu sana wakati wa hotuba yake kwa waumini Jumapili mjini Vatican.
Kutawazwa kwa Daswa kuwa mbarikiwa kumejiri chini ya miezi mitatu kabla ya Papa Francis kuzuru Afrika mara ya kwanza, ziara itakayompeleka Kenya, Uganda na Jamhuri ya Afrika ya Kati mwishoni mwa Novemba.
No comments
COMMENT