SAMATA SILAHA YA STARS
Alifunga magoli 16 katika ligi daraja la kwanza Tanzania Bara mwaka 2008 wakati akiwa na miaka 16 tu. Mwaka mmoja baadae akafunga magoli sita wakati alipocheza ligi kuu Bara kwa mara ya kwanza msimu wa 2008/09 akiwa na timu ya African Lyon.
Mbwana Samatta alipanda chati ghafla mara baada ya kuanza kuichezea Simba SC katika michezo ya mzunguko wa pili katika ligi kuu bara msimu wa 2010/11. Alifunga magoli nane
katika gemu 12 za ligi na magoli mengine matatu katika gemu nne za klabu bingwa Afrika.
Samatta ni mshambulizi hatari, ana uwezo wa dribbling kwa kasi, kupiga chenga, mashuti na uwezo wa kutengeneza nafasi za magoli. Alisajiliwa na TP Mazembe Mei, 2011 na akawa maarufu zaidi jijini Lubumbashi wakati alipofunga magoli sita katika michuano yake ya kwanza ya ligi ya mabingwa Afrika mwaka 2012 wakati TP ilipofika hatua ya nusu fainali.
Samatta aliondoka Tanzania akiwa na miaka 18 na hadi sasa amecheza zaidi ya mechi 103 na kufunga mara 60 katika timu hiyo bingwa mara nne wa kihistoria barani Afrika. Huyu ni mchezaji wa kiwango cha dunia tena bahati anatoka nyumbani Tanzania.
Amekuwa sehemu ya wachezaji wa timu ya Taifa Stars tangu mwaka 2011 wakati alipoitwa na kufunga katika mchezo wake wa kwanza wa kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika, AFCON 2012. Alifunga magoli mawili katika harakati hizo za Stars ambazo zilishindwa kufanikiwa. Akiwa tayari ameichezea Stars mara 27, rekodi ya Samatta katika ufungaji si nzuri akiwa na Stars. Ameifungia Stars mara tisa tu.
Kila inapofika mechi ya Stars wapenzi wa mpira nchini wamekuwa na matarajio ya kumuona mfungaji wao wa mipira ya kichwa na mashuti akifunga lakini mambo yamekuwa tofauti. Atakuwa anafuatiliwa kila kitu na benchi la ufundi la Nigeria na watamuandalia mikakati mikubwa kuhakikisha wana mzima.
Dhidi ya Nigeria itakuwa mechi ya kipekee kwake kwani anacheza na timu ambayo Ahmed Musa yupo. Samatta, 23, alishakwenda CSKA Moscow ya Urusi kwa ajili ya kufanya majaribio wakati Musa ndiye staa wa sasa wa ufungaji katika klabu hiyo ya Urusi.
No comments
COMMENT