AME ALLY NIRIJARIBU YANGA MAXIMO AKANIKATAA
Mshambulizi wa Azam FC, Ame Ally ‘Zungu’ amefanya mahojiano marefu na mtandao huu na kuelezea historia yake ya uchezaji. Hakika wachezaji wengi wa Kitanzania wamekutana na changamoto nyingi kabla ya kupata umaarufu. Ame alipumzika kucheza mpira kwa vipindi viwili tofauti kutokana na hali ya kimaisha lakini mchezaji huyo aliyeanza kucheza ligi kuu bara msimu uliopita alianza maisha yake ya mpira wa ushindani katika klabu ya Duma FC ya Pemba mwaka 2010.
Alicheza kwa misimu miwili kisha akapumzika kucheza mpira kwa mwaka mmoja kabla ya kurejea tena uwanjani na kujiunga na timu ya Chuoni FC ambayo aliichezea hadi aliposajiliwa na Mtibwa katikati ya mwaka 2014.
“Nilikutana na changamoto za mpira ndiyo maana kuna wakati nilipumzika kucheza mpira. Unaweza ukawa unacheza mpira lakini mwisho wa siku maisha yanaendelea kuwa magumu. Niliacha kwa muda na kugeukia upande mwingine ili kukabiliana na maisha lakini huko pia mambo yalikuwa magumu zaidi nikaamua kurudi tena katika mpira mwaka 2013 baada ya kuona nina nguvu”.
Anaanza kusema straika huyo aliyefanya vizuri msimu uliopita akiwa Mtibwa Sugar ya Turiani, Morogoro. Ame amecheza ligi daraja la Pili Zanzibar mwaka 2007 kisha akapumzika kwa mwaka mmoja na kujiunga na timu ya daraja la kwanza mwaka 2009. Alichezea Duma kisha Chuoni kabla ya kuja Dar es Salaam kujaribu maisha ya mpira. Alikwenda Simba SC lakini akapelekwa timu ya pili ( Simba B) kwa majaribio mwaka uliopita.
No comments
COMMENT