UNITED YAMKOSA ROONEY KWENYE MECHI YA UEFA
Mshambuliaji wa Manchester United Wayne Rooney ameachwa nje ya kikosi kitakachocheza mechi ya Ligi ya Kilabu Bingwa Ulaya Jumanne ugenini PSV Eindhoven kwa sababu ya jeraha.
Rooney, 29, hakucheza kwenye mechi yao dhidi ya Liverpool Jumamosi baada yake kuumia misuli ya paja akifanya mazoezi. Kilabu hiyo ya Old Trafford ilishinda 3-1 kwenye mechi hiyo.
Mkufunzi mkuu wa Red Devils Louis van Gaal alisema kulikuwa na shaka kuhusu mchezaji huyo baada ya mechi hiyo, na sasa amesema ameamua kutobahatisha.
Mshambuliaji James Wilson na kiungo wa kati Andreas Pereira wamejumuishwa kikosini.
Wawili hao hawajacheza mechi yoyote msimu huu, na majuzi Wilson alihusishwa na kuhamia kilabu inayocheza ligi ya daraja la pili kwa mkopo.
Pereira naye amechezea klabu hiyo mechi mbili pekee akiingia kama nguvu mpya, tangu ajiunge nao kutoka PSV Agosti mwaka jana.
Mechi hiyo ya Ligi ya Kilabu Bingwa Ulaya itakayochezwa Jumanne uwanja wa Phillips itakuwa ya kwanza kwa Manchester United kwenye kampeni yao Kundi B.
No comments
COMMENT