SHAMBULIO LA UA WATU 12 MSIKITINI YEMEN
WATU 12 wamefariki kwenye shambulio la bomu katika msikiti mmoja mji mkuu wa Yemen, Sanaa, maafisa wa usalama wamesema.
Shambulio hilo la kujitoa mhanga lilitokea katika mskiti wa al-Balili wakati wa swala ya Eid al-Adha.
Limejiri siku mbili tu baada ya Rais wa Yemen Abdrabbuh Mansour Hadi kurejea mji wa kusini wa Aden kutoka uhamishoni Saudi Arabia.
Alitoroka taifa hilo Machi kufuatia mashambulizi ya wapiganaji wa Houthi, ambao tangu wakati huo wamekuwa wakishambuliwa na majeshi ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia.
Muungano huo, ukishirikiana na wanajeshi wa taifa hilo, umefanikiwa kuwafurusha wapiganaji wa Houthi kutoka maeneo mengi, ukiwemo mji wa Aden.
Hata hivyo, waasi hao kutoka dhehebu la Shia, bado wanadhibiti mji mkuu.
Msikiti wa Balili uko karibu sana na chuo cha mafunzo ya polisi Sanaa. Watu wengi wanaripotiwa kujeruhiwa kwenye shambulio hilo.
Mji wa Sanaa umekuwa ukishuhudia mashambulio ya mara kwa mara ya mabomu, ambayo kundi la Kisunni la Islamic State limekuwa likidai kuhusika.
Hakuna aliyekiri kuhusika kwenye shambulio hilo la leo.
No comments
COMMENT