RAIS MAGUFULI ATOA ONYO KALI KWA WAZIRI MWIJAGE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli ameeleza kutoridhishwa kwake na hatua zinazochuliwa na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji dhidi ya watu waliouziwa viwanda na kisha kuvitelekeza huku akimtaka Waziri wa wizara hiyo Mhe. Charles Mwijage kuvinyang’anya na kuwapatia wawekezaji wanaoweza kuviendeleza.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi katika Kata ya Maweni jijini Tanga wakati wa sherehe za kuweka jiwe la ufunguzi wa kiwanda cha saruji cha Kilimanjaro.
“Hivi wewe waziri mwenye dhamana kwa nini kila wakati nasikia na kuona viwanda mbalimbali vikifunguliwa, lakini nashangaa kwa sababu sijasikia viwanda visivyozalisha vikifutwa kama anavyofanya mwenzako wa Wizara ya Ardhi kufuta hati za umiliki wa ardhi za mashamba mkubwa? Sasa nakuomba kwa mara ya mwisho hebu fumba macho na uwakung’ute,” alisema Dk Magufuli
“Mimi ndiye niliyekuteua kushika dhamana hii ya viwanda na biashara, sasa unaogopa nini? Kuanzia sasa nataka nisikie watu wamenyang’anywa, hatuwezi kuendelea kuacha maeneo hayo ya wananchi ambayo watu wameuziwa kwa bei mdogo na kuyatelekeza. Nenda kawatoe, usijali hata kama mmiliki ni kutoka CCM wewe nyang’anya, ikiwa ni mwanachama wa CUF, Chadema awe ni waziri au mbunge wewe nyang’anya,” aliongeza Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli alitoa mfano kuwa “Kwa mfano, hapa Tanga kwenye taarifa yenu hapa imeeleza kwamba kuna viwanda kumi na mbili vilivyobinafsishwa vyote havifanyi kazi, sasa wakati umefika kwamba lazima viwanda virejeshwe serikalini ili wakuu wa mikoa wakabidhi wawekezaji wengine wanaohitaji kufanya uzalishaji.”

No comments

COMMENT

All rights are recieved.. Powered by Blogger.