SERIKALI KUREJESHA DENI LA SHILINGI BILIONI 3.2 ZA SHIRIKA LA POSTA

Serikali imeahidi kuwa italirejeshea Shirika la Posta Tanzania kiasi cha shilingi bilioni 3.2, ambazo zilitumika kuwalipa wastaafu wa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki, punde ifikapo tarehe 30, mwezi Juni mwaka huu.
Ahadi hiyo imetolewa Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge wa Ludewa, Mhe. Deo Ngalawa (CCM), aliyehoji,
Serikali ilikuwa na mpango gani wa kuwalipa Wastaafu hawa yenyewe, moja kwa moja bila ya kutumia fedha za mfuko wa Shirika hilo?. Huku mbunge huyo akitaka kujua kwanini Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mwaka 2016 ilifungia akaunti za Shirika la Posta Nchini, kutokana na kulidai Shirika hilo kiasi cha Shilingi Milioni 600, ikiwa Shirika hilo linaidai Serikali kiasi cha Shilingi Bilioni 5.
Dkt. Kijaji alisema watumishi wote wa Shirika hilo wamekwisha jiunga na mifuko ya Hifadhi ya Jamii, na wanachangia katika mifuko mbalimbali hivyo wakistaafu mifuko hiyo itakuwa ikiwalipa mafao yao na si Serikali tena. Huku akiongeza kwa kusema kuwa Serikali itaendelea kulipa madeni hayo kadri fedha zitakapopatikana, watahakikisha ifikapo Juni 30 mwaka huu fedha zote zinazodaiwa na Shirika hilo zitakuwa zimelipwa.
Mhe. Ngalawa katika swali la msingi , alitaka kujua mpango wa Serikali wa kulirejeshea Shirika hilo fedha ambazo lilitumia kuwalipa Wastaafu waliokuwa Shirika la Posta na simu la Afrika Mashariki, kunusuru Shirika hilo.
Akijibu hoja hiyo Dkt. Kijaji alisema, “Shirika limekuwa likitumia fedha zake kuwalipa Wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki, huku ikiwasilisha madai Serikalini ili lipate kurejeshewa fedha zake.”
“Hadi sasa Shirika limelipa Shilingi Bilioni 5.9 na Serikali imesharejesha kiasi cha Shilingi Bilioni 2.7, alisema malipo hayo yamekuwa yakilipwa kwa awamu ambapo kwa mwezi Novemba 2016 kiasi cha Tsh. Milioni 700,000,000 zililipwa, na Disemba 2016 Tsh. 1,000,000,000 zililipwa, na Januari 2017 Sh. 1,000,000,000 zililipwa.
Aidha Dkt. Kijaji amesema Serikali itaendelea kurejesha kiasi kilichobaki cha Shilingi bilioni 3.2 kadri fedha zitakavyopatikana

No comments

COMMENT

All rights are recieved.. Powered by Blogger.